Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amefafanua kuhusu mipango ya Taifa Stars kucheza michezo ya kirafiki, akisema hatua hiyo imefanyika kwa kuzingatia mahitaji ya kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi.
Karia amesema mchezo wa kirafiki dhidi ya FAR Rabat uliopangwa kuchezwa leo ni sehemu ya maandalizi ya kocha Gamondi, ambaye alitaka kuwapa nafasi wachezaji wengi zaidi katika kikosi cha Taifa Stars kupata muda wa kucheza.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Karia alisema Gamondi alihitaji kuhakikisha hakuna mchezaji anayerejea bila kupata nafasi ya kuonesha uwezo wake uwanjani.
“Mechi tunayocheza na FA Rabat mwalimu aliitaka na ilipangwa lazima tarehe 2 ichezwe, ikiwa dhidi ya klabu au hata U23 ya Morocco, ili kuwapa wachezaji nafasi. Hakutaka kurudi na mchezaji hajacheza,” alisema Karia.
Taifa Stars inatarajiwa kushuka dimbani leo dhidi ya FA Rabat katika mchezo wa kirafiki wa ndani, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi hicho.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, Taifa Stars pia inatarajiwa kucheza mchezo mwingine wa kirafiki Oktoba 5.
Michezo hiyo inalenga kumpa Gamondi nafasi ya kuwaona wachezaji wake kwa vitendo na kufanya tathmini ya kikosi kabla ya majukumu yanayofuata ya Taifa Stars.