Kagera Sugar imefanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi baada ya kumtambulisha Amri Kiemba na Frank Domayo kuwa makocha wasaidizi wa timu hiyo kwa msimu wa 2026/27.
Kiemba ameteuliwa kuwa Kocha Msaidizi Namba Moja, wakati Domayo, aliyewahi kuitumikia Yanga SC, Azam FC na Timu ya Taifa kama mchezaji, ameteuliwa kuwa Kocha Msaidizi Namba Mbili. Wawili hao watafanya kazi chini ya Kocha Mkuu Cedric Kaze .
Uteuzi huo unafanyika wakati Kagera Sugar ikiwa imerejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Championship msimu uliopita. Klabu hiyo sasa inalenga kujenga kikosi kitakachokuwa na uwezo wa kushindana katika msimu mpya.

Kagera Sugar ilishuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2024/25 baada ya kumaliza katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 23, hivyo kuimarishwa kwa benchi la ufundi kunaweka msingi wa maandalizi ya klabu hiyo katika kurejea kwake Ligi Kuu.
Kiemba na Domayo sasa wanatarajiwa kushirikiana na Kaze Cedric katika maandalizi ya timu, huku klabu hiyo ikilenga kuwa na mwanzo mzuri na kujenga msimu wenye ushindani zaidi.