Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema timu hiyo inatarajia kufanya baadhi ya mabadiliko katika kikosi chake kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Madagascar.
Gamondi amesema mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha kiwango cha timu na kuongeza ufanisi katika eneo la ushambuliaji, huku akisisitiza umuhimu wa Taifa Stars kupata nafasi za kufunga magoli.
“Tutafanya baadhi ya mabadiliko kwenye kikosi na tunatumaini tutaonesha kiwango bora na kufunga magoli. Tuliwatazama Madagascar kwenye mchezo wao dhidi ya Nigeria, ni timu nzuri sana, itakuwa mechi ngumu.”
Kocha huyo amesema Madagascar ni timu yenye uwezo, baada ya kupata nafasi ya kuifuatilia katika mchezo wake dhidi ya Nigeria.
Kwa mujibu wa Gamondi, maandalizi ya Taifa Stars yamezingatia uwezo wa mpinzani wao, huku akitarajia mchezo huo kuwa na ushindani mkubwa.
Macho ya mashabiki wa Tanzania sasa yanaelekezwa kwenye mchezo huo, huku Taifa Stars ikitakiwa kuonyesha kiwango bora na kutumia vizuri nafasi zitakazopatikana mbele ya lango la Madagascar.