Kocha mkuu wa klabu ya Raja Club Athletic, Fadlu Davids, yuko mbioni kuondoka katika klabu hiyo baada ya pande zote mbili kuanza mazungumzo ya kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, kikao kilichofanyika jana kati ya uongozi wa Raja CA na kocha huyo wa Afrika Kusini hakikufikia muafaka wa mwisho kuhusu masharti ya kuachana. Kikwazo kikubwa kimeendelea kuwa suala la fidia ya kuvunjwa kwa mkataba.
Inaelezwa kuwa Raja CA wanatarajiwa kulipa kiasi cha dola za Kimarekani 215,000 ili kusitisha mkataba wa Davids, huku mazungumzo yakiendelea ili kufikia makubaliano ya mwisho.
Pande zote mbili zinatarajiwa kukutana tena katika juhudi za kumaliza mchakato huo na kufikia mwafaka rasmi.
Ingawa hadi sasa hakuna hati yoyote iliyosainiwa rasmi, dalili zote zinaonyesha kuwa kuondoka kwa Davids katika klabu hiyo ni suala la muda tu.
Davids alichukua mikoba ya kuinoa Raja CA baada ya kuondoka Tanzania, ambako aliwahi kufanya kazi katika benchi la ufundi la Simba SC.
Raja CA imefikia uamuzi wa kumfuta kazi baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo matokeo yaliyopelekea timu hiyo kushuka hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi tofauti ya alama nne dhidi ya vinara wa ligi RS Berkane.



