Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB , iliyopangwa kufanyika Uwanja wa Tanzanite, Babati mkoani Manyara, itazikutanisha Azam FC na Mabingwa Watetezi, Yanga kama ilivyokuwa msimu uliopita
Hii ni baada ya Yanga jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
Juzi Azam Fc ilishuhudiwa ikitangulia fainali ya michuano hiyo kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba
Jana ilibidi Yanga isubiri hadi dakika ya 100 ili kupata bao baada ya mechi hiyo kuingia kwenye dakika 120 kufuatia dakika 90 kumalizika bila kufungana
Bao hilo lilifungwa na kiungo, Stephane Aziz Ki kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya kupokea pasi ya Pacome Zouzoua aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli
Mpira ulianzia kwa Khalid Aucho aliyemnyang'anya mchezaji mmoja wa Ihefu na kuipeleka wingi ya kulia ambako Pacome alikuwapo, akaingia ndani kidogo na kumtengea mfungaji wa bao
Fainali hiyo itakuwa inajirudia tena kwani msimu uliopita timu hizo zilikutana Juni 12, mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa wavuni na Kennedy Musonda
Katika mechi mbili za ligi kuu ambapo timu hizo zilikutana msimu huu kila moja ilishinda mechi moja. Yanga ilishinda mabao 3-2 katika mchezo wa duru ya kwanza na Azam Fc kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa duru ya pili
Itakuwa mechi nyingine ya fainali inayotarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake