Kocha Mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha amesema kikosi chake kilikuwa na nafasi ya kushinda mchezo dhidi ya Wydad Casablanca uliopigwa juzi nchini Morocco lakini wachezaji wake walikosa umakini katika umaliziaji
Simba ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 1-0 wakiruhusu bao kwenye dakika za lala salama
Benchikha amesema wachezaji walicheza vizuri kwa muda mwingi wa mchezo ikiwa ni pamoja na kutengeneza nafasi adimu ambazo hawakuzitumia
"Nafikiri tulikuwa na nafasi nzuri ya kushinda mchezo huu kwa kuzingatia nafasi tulizotengeneza lakini tulikosa ukatili katika eneo la umaliziaji"
"Tumecheza vizuri, tuliweza kuzuia na kushambulia kwa kasi, eneo la kuweka mpira nyavuni ndilo tumeshindwa kufanikisha lakini nimeridhishwa na timu ilivyocheza"
"Yote yaliyotokea hapa yatakwenda kutupa usahihi wa maandalizi mazuri ya mchezo ujao. Eneo tulilokuwa bora tutakwenda kuongeza ili kuimarika zaidi na kwenye mapungufu tutakwenda kuparekebisha," alisema Benchikha
Kikosi cha Simba kiliondoka Morocco jana wakipitia Qatar kurejea nchini ambapo Ijumaa ya wiki hii wanakabiliwa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa uwanja wa Uhuru