Kocha wa Al Ahly Pitso Mosimane amesema mchezo mgumu zaidi ambao wamecheza mpaka sasa kwenye Caf Champions League msimu huu ni ule dhidi ya Simba Sc nchini Tanzania
Al Ahly wametinga fainali ya mashindano hayo kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuifunga Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-0 katika nusu fainali
Watamenyana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika fainali Julai 17 huko Casablanca, Morocco
Katika moja ya mahojiano yake alipoulizwa mchezo mgumu aliokumbana nao kwenye michuano hiyo hadi sasa, alichagua ule dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao Simba ilishinda kwa bao 1-0
"Nadhani mchezo dhidi ya Simba katika hatua ya makundi Tanzania ulikuwa mgumu zaidi. Wenzetu waliruhusiwa kuingiza mashabiki jambo ambalo hatuwezi kulalamika juu yake lakini hatukutarajia. Tulicheza muda ambao haukuwa rafiki kwetu, angalia picha zilizopigwa nchini Tanzania, ilikuwa ngumu sana," alisema
Mchezo dhidi ya miamba ya Msimbazi ulikuwa wa pili kwa Al Ahly katika hatua ya makundi na bao lililofungwa vizuri kutoka kwa winga wa Msumbiji Luis Miquissone lilitosha kuwapa ushindi kuwapa Simba ushindi muhimu uliowafanya wajikite kileleni mwa kundi A
Simba ilimaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi A na kutinga robo fainali ambako kwa bahati mbaya hesabu hazikutimia kuweza kuivusha Simba hatua ya nusu fainali
Lakini ni wazi kwa michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu, Simba ilistahili kufika mbali zaidi