Licha ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania juzi, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema walichokuwa wanakihitaji ni pointi tatu tu na si idadi kubwa tena ya mabao kwa kuwa kwa upande huo wana mtaji wa kutosha
Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 70 na mabao 65 ya kufunga na 11 ya kufungwa baada ya kushuka dimbani mara 28, huku Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 67 na mabao 49 ya kufunga na 22 ya kufungwa, yaliyotokana na michezo 31
Azam inafuata katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 63 na mabao 48 yakufunga na 21 ya kufungwa baada ya kushuka dimbani mara 31 kwenye ligi hiyo inayojumuisha timu 18 msimu huu.
Akizungumza baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Simba ikipata ushindi huo kupitia faulo iliyopigwa na Luis Miquissone, Matola alisema haiwezekani kila mechi timu icheze kama inavyokuwa siku zote na hasa ukichukulia kuwa wachezaji wengi wametoka kwenye mapumziko ya mechi za Kalenda ya FIFA za timu za taifa.
"Tumepata pointi tatu. Hicho ndicho kikubwa. Kama nilivyosema mwanzo kabla ya mechi kuwa hautokuwa mchezo rahisi, hasa sisi tukikutana na Polisi Tanzania, huwa mechi ngumu, japo mechi zote nne tulizocheza nao tumeshinda. Tunashukuru kwa tulichokipata kwa sababu haiwezekani timu ikacheza vizuri kila siku," alisema Matola.
Ili kuifikia Simba kwa mabao, Yanga watalazimika kufunga mabao 27 katika michezo mitatu iliyobaki na hata Azam Fc nao watahitaji idadi hiyo ya mabao
Kwa wastani timu hizo zinapaswa kushinda 9-0 katika kila mchezo na moja ya mechi hizo ni dhidi ya Simba
Na hapa ndio maana Simba inahitaji kushinda mechi mbili tu kufikisha alama 76 ambazo kimahesabu Yanga wanaweza kufikisha lakini hawataweza kufikisha idadi ya mabao ambayo Simba anayo