Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes anatarajiwa kurejea leo nchini akitokea kwao Ufaransa kwa mapumziko mafupi, tayari kwa ajili kukiongoza kikosi chake kuelekea mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA
Meneja wa mabingwa hao wa nchi, Patrick Rweyemamu, alisema Gomes atawasili leo muda wowote kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake wakilenga kutetea mataji yao, Ligi Kuu na Kombe la FA.
"Kocha wetu anatarajiwa kuwasili hapa nchini kesho (leo), muda wowote kuendelea na majukumu ya kuinoa timu yetu ambayo inajiandaa na michezo ya Ligi Kuu pamoja na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam," alisema Rweyemamu.
Meneja huyo alisema timu yao inaendelea na mazoezi ikiwa na wachezaji ambao hawajaitwa katika timu zao za taifa.
Mbali na kutinga nusu fainali ya Kombe la FA, pia Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 67, sita mbele ya Yanga inayoshika nafasi ya pili na ikiwa mbele michezo miwili.