Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu klabu ya Simba Suleiman Kova amesema mapendekezo waliyotoa kwa uongozi kuhusu shauri la kiungo Jonas Mkude yamelenga kumsaidia mchezaji huyo
Baada ya Kamati ya Nidhamu kumuhoji Mkude kwa mara ya pili mwaka huu kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu, kabla ya kutoa hukumu, Kamati imependekeza apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi
"Mkude amekabiliwa na makosa yanayojirudia. Sasa tumeona ipo haja ya mchezaji huyu kusaidiwa kwa kuwashirikisha wenzetu wa kada nyingine kubaini tatizo lake hasa nini kabla kumuhukumu"
"Hii sio mara kwanza anafikishwa kwenye Kamati yetu kwa makosa haya haya, " alisema Kova
Mkude alifikishwa mbele ya Kamati hiyo mwanzoni mwa mwaka huu akituhumiwa na makosa ya utovu wa nidhamu
Alipewa adhabu ya kusimamishwa pamoja kukatwa sehemu ya mshahara wake pia akiwekwa katika uangalizi maalum
Lakini makosa haya sasa yamezoeleka kwa Mkude. Wakati wa kocha Joseph Omog Mkude alinyan'ganywa unahodha na jukumu hilo kupewa John Bocco wakati timu iko kambini Afrika Kusini baada ya kufanya utovu wa nidhamu
Alikumbana na adhabu hata walipokuwepo makocha Patrick Aussems na Sven Vandenbroeck
Sio katika klabu tu, hata kwenye timu ya Taifa, Emmanuel Amunike alimuacha katika kikosi chake kilichoshiriki michuano ya Afcon 2019
Etienne Ndayiragije nae mara kadhaa alilamika huku Kim Poulsen akimuacha nje katika kikosi chake kitakachocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi wiki ijayo
Ni uamuzi busara sana uliochukuliwa kuwashirikisha wataalam wa Afya kubaini changamoto zinamkabili Mkude ili kuokoa kipaji chake
Mkude anapaswa kutoa ushirikiano katika hili kwani mwisho wa siku, mnufaika wa kwanza ni yeye