Mabingwa wa nchi Simba wako jijini Mwanza wakisubiri mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting, itakayopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba kesho huku Kocha Mkuu Didier Gomes, akisema wanachohitaji ni kutetea ubingwa wao mapema na si vinginevyo
Simba itashuka dimbanni kesho ikitaka kuendeleza kasi yake ya ushindi kwenye viporo vyake baada ya Jumamosi kutoka kuibabua Namungo FC mabao 3-1 katika mechi ya ligi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Gomes, amesema kwao kila mchezo ni muhimu kushinda na anahitaji kuona wakiibuka na ushindi mbele ya Ruvu Shooting ili kufikia malengo yao jambo linalowafanya wawe na hesabu kali kila wanaposhuka uwanjani.
Alisema wana mechi nyingi za kucheza kwa sasa, hali ambayo inawalazimu kuongeza umakini na tayari hesabu zao wamezielekeza kuvuna pointi tatu dhidi ya Ruvu Shooting.
"Mechi ya kwanza tulipoteza mbele ya wapinzani wetu hao, sasa hatutaki kurudia makosa ya awali, utakuwa ni mchezo wa ushindani mkubwa na mgumu kwa sababu tunahitaji kuvuna pointi tatu kwao kama ambavyo nao wanahitaji"
"Kikubwa tunachohitaji ni ushindi tu katika mchezo huo, ila tunawaheshimu wapinzani wetu, hivyo tutaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ya kwenda kutafuta matokeo chanya," alisema Gomes.
Alisema ana matumaini makubwa na wachezaji wake kufanyia kazi yale anayowapa katika mazoezi na kuonyesha uwanjani kwa sababu amekuwa akiridhishwa na jinsi ambavyo nyota wake hao wanavyopambana katika kila mechi na kupata ushindi.
"Tunahitaji sana ushindi ili kufikia malengo yetu ya kutetea ubingwa, nina imani kubwa na vijana wangu kufanikisha kile ambacho mashabiki na Wanasimba wanakitarajia mwishoni mwa msimu huu"