Kiungo wa Simba Hassan Dilunga amemshukuru kocha Didier Gomes kumuamini na kumpa nafasi katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc juzi Jumamosi
Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, Dilunga alihusika katika mabao yote
Dilunga alikuwa katika kiwango bora sana, aliwanyamazisha wale waliokuwa wanahoji kwa nini alijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa kabla ya jina lake kuondolewa muda mfupi baadae
Dilunga alisema Gomes alimuamini ndiyo maana baada ya mpango wa kwanza kushindwa, alimpa nafasi kwa ajili ya mpango wa pili ambao alichangia kufanikiwa.
"Mchezaji kukaa nje si kama ni mbovu, hujui au huna kiwango. Inawezekana umewekwa kwa sababu ya plan ya pili ya kocha. Na mimi kama mchezaji si kama ukiwekwa nje basi ubweteke, nafanya mazoezi kwa bidii, mambo ya kucheza anajua mwalimu, siku akimua akuingize uwanjani ukafanye kazi, basi unakuwa fiti unakwenda kufanya kazi kama ilivyokuwa kwenye mechi hii. Kwa hiyo kocha wetu nampongeza kwa hilo," alisema Dilunga
Mchezaji huyo alikataa kuzungumzia sintofahamu ya jina lake kutajwa kwenye timu ya taifa, akisema kuwa kwa sababu walikosea kulitaja jina lake, basi hata yeye anaamini kuwa walikosea tu na si maana nyingine yoyote inayotafsiriwa.
Dilunga amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi katika kila mechi kama ilivyokuwa kwenye mechi hiyo hadi siku ya kutangazwa kuwa bingwa