Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amemtolea uvivu Patrick Gakumba ambaye ni Wakala wa mshambuliaji Meddie Kagere kuwa hana haki ya kuingia majukumu ya kocha Didier Gomes
Hivi karibuni Gakumba amenukuliwa na vyombo vya habari akimshushia lawama kocha mkuu wa Simba Didier Gomes kuwa ana chuki na Kagere kwa kuwa yeye (Gakumba) aliwahi kumnyima nafasi ya kuinoa moja ya nchi alizokuwa akizisimamia
Manara amemtaka Gakumba ajitathmini kwani anavuka mipaka ya majukumu yake

"Nafikiri sasa kazi ya Mawakala haiendeshwi vile inavyotakikana. Kazi ya Wakala ni kusimamia maslahi ya mteja wake na si vinginevyo. Suala la mchezaji kucheza liko chini ya kocha mwenyewe. Sisi viongozi wa klabu hatupaswi kuwaingilia makocha, yeye Wakala ni nani?," alihoji Manara
"Anazungumzia Kagere kunyimwa nafasi mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs juzi, pengine hata hafahamu sheria mpya ya 'substitution'. Mchezo dhidi ya Kaizer tulilazimika kufanya mabadiliko mara mbili kwa dharura"
"Pamoja na kuwa tulikuwa na ruhusu ya kufanya mabadiliko ya wachezaji mpaka watano, lakini sheria inataka ufanye mabadiliko hayo katika mikupuo mitatu tu. Sasa tayari tulikuwa tumemtoa Mzamiru, baadae tukalazimika kuwatoa Onyango na Lwanga ambao waliumia. Hatukuwa na nafasi nyingine ya kufanya mabadiliko"
"Tunamuheshimu sana Gakumba lakini tunamuomba asiingilie mambo ya benchi la ufundi, yeye abaki katika jukumu la kutetea maslahi ya mchezaji wake tu," alisema Manara
Ni wazi Gakumba anaweza kumuharibia Kagere akidhani anamtetea kwani uongozi wa Simba hautakuwa tayari kuendeshwa na Wakala ambaye kauli zake zinaweza kusababisha mgogoro baina ya mchezaji na benchi la ufundi