Jioni ya leo Jumamosi May 22, mabingwa wa soka Tanzania Simba watashuka katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuumana na Kaizer Chiefs katika mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Hii ni siku iliyosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Simba na Watanzania wazalendo wanaofahamu manufaa ambayo nchi inapata kwa Simba kufanya vizuri
Aidha, ni mchezo ambao Simba inasaka kuandika historia nyingine kutokana na aina ya matokeo wanayopaswa kuyapata
Simba wataingia katika mchezo huo wakiwa nyuma kwa mabao 4-0 baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa idadi hiyo ya mabao Afrika Kusini
Hivyo Simba inahitaji kushinda sio chini ya mabao matano kuweza kutinga nusu fainali
Wakati akizungumza na wanahabari katika mkutano kuelekea mchezo jana, Mkufunzi wa Simba, Didier Gomes alisema wachezaji wana ari na morali ya 'kupindua meza'
Alisisitiza kuwa hakuna jambo lilsilowezekana kwenye mpira wa miguu na wamejipanga kushinda mchezo huo kwa gharama yoyote
Hii ni nafasi nyingine kwa wachezaji kuipaisha Simba Kimataifa, kwani kama watafanikia kutinga nusu fainali, Afrika yote itakuwa ikiizungumza Simba
Sifa hii pia itarudi kwa Tanzania na ligi yetu itazidi kupanda thamani
Mashabiki 10,000 watakaoingia uwanja wa Mkapa leo watakuwa na kazi moja tu, kushangilia kwa dakika zote 90 za mchezo kuwahamasisha wachezaji
Huwezi kuitenganisha Simba na mashabiki wake, hamasa ya mashabiki imekuwa chachu kubwa kwa Simba kufanya vizuri katika michezo yake yote inayochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Hii ni siku ya kuweka historia, hii ni siku ya kufa au kupona kwa Wanasimba. Ni ama zao ama zetu...!