Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara ametangaza viingilio vya mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ambao utapigwa Jumamosi May 22 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam
Manara amesema Simba imedhamiria kuvuka nusu fainali hivyo wamejipanga kupata ushindi wa mabao matano dhidi ya Chiefs
Kauli mbiu kuelekea mchezo huo ni ama zao ama zetu, 'Do or Die season 2

Manara amesema mpaka sasa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetoa ruhusa ya mashabiki 10,000 kuingia uwanjani hivyo amewataka Wanasimba kuchangamkia tiketi mapema
"Tuna nafasi 10,000 mkononi, tumewaomba CAF watuongezee nafasi zaidi , tunaanza kuuza tiketi leo kwa hawa 10,000 tulionao kwanza"
"Viingilio VIP A ni Tsh 40,000/- VIP B na C ni Tsh 25,000/- na Mzunguuko ni Tsh 5,000/- . Pia tutakuwa na tiketi za Platinums ambazo zitauzwa kwa Tsh 150,000/-"
Manara amesisitiza kuwa Simba itashinda mchezo wa Jumamosi na kutinga nusu fainali
"Tunajua Wanasimba wanataka kufuzu, hatutaki kujitahidi, Simba sio timu ya kujitahidi, ni timu ya kufuzu. Mashabiki wanaiamini timu yao inaweza."
"Kama uongozi tumejiandaa na mchezo wa jumamosi. Tunaamini wachezaji watapokea maelekezo vizuri kutoka kwa walimu na tutashinda."
"Mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa mpya wa Dar es Salaam, Amos Makala. Tunakukaribisha kaka yetu Makala, utuongozee Wanasimba kushangilia."