Mratibu wa Simba Abbas Ali amewataka mashabiki kutokata tamaa kwani wanajipanga kuwapa furaha kwenye mchezo wa marudiano robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya Kaizer Chiefs
Baada ya mapumziko ya siku moja, kikosi cha Simba kimeingia kambini leo kuanza maandalizi ya mchezo huo wa mkondo wa pili utakaopigwa May 22 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Pamoja na Simba kuhitaji kufunga zaidi ya mabao manne ili kuweza kutinga nusu fainali, Abbas amesema kwenye mpira wa miguu lolote linawezekana
"Tumerejea kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Kaizer Chiefs. Tulipoteza mchezo wa kwanza ugenini nasi tuna nafasi ya kushinda nyumbani. Tunawambia mashabiki wetu wasikate tamaa kwani tumedhamiria kushinda mchezo huo. Kama wao wametufunga kwao nasi tinaweza kuwafunga kwetu"
"Tunasubiri maombi tuliyopeleka CAF kuhusu mashabiki kuingia uwanjani, kama tutaruhusiwa tunawaomba waje kwa wingi kutuunga mkono," alisema Abbas
Simba itahitaji kushinda angalau mabao matano ili kuweza kutinga nusu fainali moja kwa moja