Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara ameeleza jinsi alivyopata wakati mgumu nchini Afrika Kusini mwishoni mwa wiki wakati Simba ilipochuana na Kaizer Chiefs
Matokeo ya mchezo huo kwa Simba kufungwa mabao 4-0 hakuna aliyetarajia hasa ukizingatia ubora wa Simba kwenye hatua ya makundi
Ukweli ni kwamba Simba iliingia robo fainali kutoka kwenye kundi gumu ambalo lilijumuisha mabingwa watetezi Al Ahly na AS Vita
Kila mmoja alikuwa akiipa Simba nafasi ya kufanya vizuri dhidi ya wapinzani wao Kaizer Chiefs ambao hata kwenye ligi yao wanasuasua
Kwa hakika kilichotokea ni matokeo ya mchezo ambayo yamewaumiza wanasimba wengi
Manara amesema hakuweza kuushuhudia mchezo huo mpaka mwisho kwani kuna nyakati hakuweza kuvumilia na kujikuta anapoteza fahamu
"Kwa kweli nilikuwa na wakati mgumu. Hali yangu ilikuwa tete, ningeweza kupoteza maisha. Nilizimia mara mbili, nina tatizo la presha ya kushuka mara nyingi huwa natumia chumvi kujiweka sawa"
"Kwa sasa nashkuru naendelea vizuri lakini huu mpira huu unaweza kutuua siku moja," alisema Manara
Pamoja na kuwa kiongozi, Manara ni Mwanasimba kwelikweli, huyu ni kiongozi wa mfano ambaye mara nyingi husimamia mambo ya klabu ya Simba kwa gharama yoyote