Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes ameeleza masikitiko yake baada ya mchezo dhidi ya Yanga uliokuwa upigwe jana katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuahirishwa kufuatia mkanganyiko wa muda wa mchezo huo
Gomes amesema kikosi chake kilikuwa kimejiandaa kikamilifu kuwapa furaha mashabiki wao. Hata hivyo kinyume na matarajio yao, mchezo haukuchezwa
Aidha Gomes amewapa pole mashabiki waliokumbwa na kadhia hivyo wakiwa wamelipa viingilio na kuingia uwanjani
"Tulikuwa tayari kwa ajili ya mchezo huu na maandalizi yalikuwa yamekamilika. Tulitamani tucheze mechi ya jana ili kuongeza utimamu kwa wachezaji wetu kuelekea mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief lakini imeshindikana hivyo tunajiandaa kwa mchezo ujao"
"Tunatoa pole kwa mashabiki na wadau waliojitokeza kwa wingi uwanjani kuja kushuhudia mchezo, ninaamini wenye mamlaka watakaa pamoja na kutafuta njia sahihi ya kutatua hili," alisema Gomes
Mashabiki wanasubiri kauli ya TFF kuhusu hatma ya fedha zao kwa wale ambao walikata tiketi kuweza kushuhudia mchezo huo uwanja wa Benjamin Mkapa
Takribani mashabiki 40,000 walikata tiketi kushuhudia mchezo huo
Kwa hakika tukio hili limechafua taswira ya soka la Tanzania ambalo tayari limeanza kufuatiliwa karibu Afrika yote kutokana na mafanikio wanayopata Simba katika michuano ya ligi ya mabingwa