Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema litaimarisha ulinzi katika mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, huku likiwaonya mashabiki kwenda uwanjani bila silaha yoyote.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unatarajia kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 6, 2021, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema hakuna ruhusa ya mashabiki kuingia na chupa za maji majukwaani kwa sababu huwa wanazitumia kama silaha pale wanapotofautiana au kuelemewa
Pia Mambosasa amewaonya mashabiki wa timu hizo kuacha kwenda uwanjani na aina yoyote ya silaha, akisisitiza kutakuwa na ukaguzi makini. Aidha amewataka wazazi na walezi wanaopenda kwenda na watoto uwanjani wakae nao karibu na wasiwaache wakatangatanga.
"Tunawatakia mashabiki kushangilia kwa amani na utulivu wawapo uwanjani na kuepuka mambo yafuatayo. mihemko na maneno ya kuhasimiana kati ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa sababu ndio chanzo cha kutofautiana na kuhama kutoka katika mchezo na mwisho kugeuka masumbwi," alisema Mambosasa
Mchezo huo ambao Simba atakuwa mwenyeji, utapigwa kuanzia saa 11 jioni