Mabingwa wa nchi Simba wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya watani zao Yanga ambao utapigwa Jumamosi, May 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Huu ni mchezo ambao Simba inahitaji alama zote tatu ili kujisafishia ubingwa wa nne msimu huu
Kuelekea mtanange huo mshambuliaji Meddie Kagere amesema wanahitaji kushinda ili kuongeza kasi katika kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne.
Kagere amefunga mabao mawili katika mechi za dabi zilizopita. Atakuwa akifukuzia rekodi ya mabao katika michezo hiyo
Pamoja na kutokuwa nafasi ya kuanza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, msimu huu amepachika mabao 11 katika ligi akishika nafasi ya pili nyuma ya Prince Dube aliyepachika mabao 12
Kagere amesema wanachokifikiria wachezaji wa Simba ni kuhakikisha wanashinda mchezo wa Jumamosi ili kujihakikishia taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini pia ni wakati sahihi wa kupambana kuhakikisha anarejea kileleni na kumshusha Dube katika orodha ya wafungaji.
"Tuko vizuri na tunaendelea na mazoezi kwaajili ya mchezo ujao, nipo hapa kwaajili ya kuipambania timu yangu pamoja na kutimiza malengo yangu ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora ingawa najua msimu huu haitakuwa rahisi kutokana upinzani uliopo hivi sasa," alisema Kagere
Kagere anafukuzia rekodi ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwa msimu wa tatu mfululizo akiibuka mfungaji bora msimu wa 2018/19 (mabao 21) na 2019/20 (mabao 22)
Kutokana na rekodi yake ya kuifunga Yanga mabao mawili, Kagere anaweza kuanzishwa katika mchezo huo wa Jumamosi