Jumamosi ya wiki hii, Machampioni wa soka Tanzania, Simba watashuka dimba la Benjamin Mkapa kuwakabili watani zao Yanga katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Huo ni mchezo wa duru ya pili baina ya timu hizo ambapo mchezo wa kwanza ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Simba iko kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa wamejikusanyia alama 61, nafasi ya pili ikishikwa na Yanga yenye alama 57
Simba ina mechi nyingine mbili za viporo ambazo kama watashinda zote wataweza kuongoza ligi kwa tofauti ya alama 10
Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes anaamini kuwa ushindi dhidi ya Yanga utawahakikishia kutetea taji lao kwa msimu wa nne mfululizo
Tangu aanze kuinoa Simba, Gomes amepata sare katika michezo miwili tu ya ligi akifanikiwa kushinda michezo yote sita iliyopita katika mashindano yote
"Sisi tupo tayari kwa mchezo dhidi ya Yanga, morali yetu ipo juu, tumetoka kucheza mechi sita na kushinda zote na mechi hii itaonyesha nani atakuwa bingwa kwa hiyo ni vizuri kushinda nayo," alisema Gomes
Katika miaka ya karibuni Simba imetawala mechi za dabi dhidi ya Yanga, matumaini ni makubwa kuwa Mnyama ataunguruma pale kwa Mkapa siku ya Jumamosi