Waliotizama mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam juzi kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Yanga, walishuhudia madudu yaliyofanywa na waamuzi katika mchezo huo
Pamoja na kunyimwa mkwaju wa penati wa wazi, nahodha wa Prisons Benjamin Asukile akafichua kuwa kulikuwa na rushwa ya Tsh Milioni 40 ambayo ilikuwa imeahidiwa na watu ambao Asukile alidai walikuwa wakiwapigia simu
'Madudu' hayo yamemuibua Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara ambaye amesema kuwa wamejipa jukumu la kuwalipia kisasi Prisons siku ya Jumamosi katika mchezo wa ligi kuu ambao watacheza na Yanga
Ahadi kama hiyo aliitoa kwa Kagera Sugar msimu uliopita na Simba kuifumua Yanga mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali ASFC
"Prisons vibweka vya juzi tutawalipia tarehe nane Inshallah, ondoeni hofu Simba ndio Bingwa wa nchi hii na tunao wajibu wa kuwalipizia wote wanaonewa!! Sisi ndio Simba wengine Mafisi," alitamba Manara
Simba imepania kutetea ubingwa wake kwa msimu wa nne mfululizo, ushindi dhidi ya Yanga utawahakikishia kushinda ubingwa mapema