Mabingwa wa nchi Simba wametoa adhabu kali kwa Mtibwa Sugar wakiifumua mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ambao umepigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Ulikuwa mchezo ambao Simba ilidhihirisha kuwa bora sana, hakika kucheza ligi kuu kwao sasa ni kama wanafanya mazoezi tu
Sio kwamba Mtibwa Sugar walikuwa wabaya, lakini Simba walikuwa bora sana, haikuwa kazi rahisi kwa Mtibwa Sugar kuwakabili vijana wa kocha Didier Gomes waliokuwa na kiu ya ushindi tangu dakika ya kwanza
Clatous Chama, Larry Bwalya na Meddie Kagere waliipeleka Simba mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0

Kagere akaongeza bao la nne katika kipindi cha pili ambacho pia alishuhudia Luis Miquissone akifunga bao la 'kideoni' akiifungia Simba hesabu ya mabao leo
Pengine yawezekana kikosi hiki cha Simba cha wakati huu ndio kikosi bora kuwahi kutokea katika historia ya Simba
Simba hii ina kila dalili ya kufanya maajabu huko kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Kwa hapa nyumbani, Simba haitakuwa na kikwazo chochote kutetea ubingwa wake