Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, wanarejea katika ligi ya nyumbani kwa nguvu ileile waliyotumia katika ligi ya mabingwa
Kocha huyo raia wa Ufaransa amesema anahitaji kuona kikosi chake kinakaa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya michezo minne inayofuata
Gomes amesema katika michezo hiyo ya ligi, kikosi alichokitumia kwenye michuano ya ligi ya mabingwa hakitakuwa na mabadiliko makubwa
Atatumia wachezaji walewale walioipeleka Simba robo fainali ya michuano hiyo huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi
"Tumemaliza majukumu ya klabu bingwa Afrika hatua ya makundi sasa tumerejea kwenye Ligi, tunataka kurejea kileleni mwa msimamo katika mechi zetu nne zijazo za mwezi huu, tutatumia wachezaji wale wale waliocheza Ligi ya Mabingwa," alisema Gomes
Simba itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumatano kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo ambao matokeo ya ushindi yatawasogeza mabingwa hao wa nchi karibu kabisa na nafasi ya kwanza kwani watahitaji alama nyingine mbili tu kutoka michezo mitatu ili kuongza ligi