Ni hivi, huwezi kulitaja soka la Tanzania bila kuitaja klabu ya Simba SC, ambayo inaipeperusha vyema bendera ya taifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamekuwa tishio zaidi sio hapa nyumbani pekee bali Afrika ambako hivi sasa ndio timu ambayo imekuwa gumzo zaidi kutokana na kuwa katika kiwango cha juu na kuwa tishio kwa klabu kubwa kutokana na ubora wao wa nje na ndani ya Uwanja.
Simba SC, wamefuzu hatua ya robo fainali ikiwa na pointi 13 kileleni mwa msimamo, rekodi ambayo itachukua muda mredu kuvunjwa na klabu za soka hapa mchini.>
TIMU PEKEE
Kwa sasa Simba ndio klabu pekee katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, kwani ndio timu pekee inayoshiriki michuano hiyo, ambayo imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Hii ni mara ya pili kwa timu hiyo kufikia hatua hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitatu, kwani iliwahi kufanya hvyo msimu wa mwaka 2018/19 na sasa 2020/21.
Hizi ni baadhi ya rekodi zilizovunjwa na kuandikwa na klabu ya Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu wa mwaka 2020/21 na kuwa gumzo kila pembe ya Afrika.
WACHEZAJI BORA
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kutoa wachezaji bora wa wiki mara mbili katika hatua ya makundi baada ya kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone kuweno katika orodha ya wachezaji bora wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
Mwingine wa Simba aliyewahi kutajwa katika kikosi bora cha wiki cha Caf ni Mzambia Clatous Chota Chama.
NYOTA WATATU
Simba wamekuwa katika kiwango bora msimu huu katika hatua ya makundi imekuwa na uwiano mzuri wa kufunga mabao tofauti na msimu wa 2018/19, ambapo nyota wake walikuwa wakifunga mabao machache.
Msimu huu hali ni tofauti safu ya ushambuliaji imeimarika katika hatua ya makundi katika orodha ya wafungaji kuna nyota watatu, Luis Miquissone ana mabao matatu, huku Chama na Chris Mugalu kila mmoja akiwa na mabao mawili.
KUFUNGWA MACHACHE
Msimu huu ni tofauti kabisa na ule wa mwaka 2018/19, kwani Simba ilimaliza hatua ya makundi ikiwa imefungwa jumla ya mabao 13, lakini msimu huu katika mechi sita imeruhusu mabao mawili tu
Simba iliifunga AS Vita mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 nchini Congo, na hivyo kuwa tofauti kabisa na misimu iliyopita, ambapo timu hiyo ilishinda mechi za nyumbani tu huku ugenini ikipokea gunia la mabao.
KUFUZU MAPEMA
Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Simba kufuzu hatua ya robo fainali ikiwa ina mchezo mkononi, lakini pia imemaliza hatua ya makundi ikiwa kileleni mwa msimamo wa Kundi A, ikiwa imejikusanyia pointi 13.
Hatua hiyo ya kufuzu huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi umeibua gumzo katika soka la Afrika na sana sana kutokana na kiwango chake ilichokionesha msimu huu.
MANULA AVUNJA REKODI
Kipa namba moja wa Simba na Tanzania, Aishi Manula amevunja rekodi ya misimu wa mwaka 2018/19 baada ya msimu huu kufungwa mabao mawili tu ndani ya mechi tano.
Msimu wa mwaka 2018/2019, Manula alijikuta katika wakati mgumu baada ya kupachikwa mabao 11 katika jumla ya mechi tano, lakini msimu huu ndani ya mechi sita ameokota mpira wavuni mara mbili tu
Lakini pia Manula mwaka huu ameweka rekodi ya kucheza michezo minne mfululizo akizuia lango lake kuguswa alifanya hivyo dhidi ya AS Vita katika ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Al Ahly waliposhinda bao 1-0, walipotoka sare ya bila kufungana na El Merrick na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya timu hiyo ya Sudan.
WANNE KIKOSI BORA
Mwaka huu umekuwa na mafanikio kwa Simba katika michezo sita imeingiza nyota wanne katika kikosi bora cha wiki cha Caf, ambao ni Joash Onyango, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Clatous Chama na Luis Liquissone, ambaye ameingia katika kikosi hicho mara tatu, lakini pia akishinda bao bora la wiki alilofunga dhidi ya Al Ahly
Aidha Chama alishinda tuzo ya mchezaji bora wa wiki baada ya mechi za raundi ya tano