Hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika imekalika kwa Simba kupoteza mchezo pekee katika hatua hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly
Ulikuwa ni mchezo wa kukamilisha ratiba tu kwa timu zote kwani tayari zilishakata tiketi ya kutinga robo fainali
Al Ahly waliotumia uwanja wao kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo msimu huu, walikuwa bora zaidi kwenye kipindi cha kwanza ambacho walikitumia kufunga bao pekee la ushindi
Kipindi cha pili Kocha Didier Gomes alifanya mabadiliko ya kiuchezaji ambayo yaliwanufaisha zaidi mabingwa hao wa nchi kwani walitengeneza nafasi ambazo kama zingetumika Simba ingesawazisha na pengine kufunga mabao zaidi
Simba imemaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi A baada ya kufikisha alama 13 wakati Al Ahly wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 11
AS Vita wamepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Merrikh na hivyo kumaliza nafasi ya tatu wakiwa na alama saba
Al Merrikh wamemaliza mkiani kundi A wakiwa na alama mbili