Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes ameeleza kufurahishwa na kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita ambao Simba ilifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 4-1 na kutinga robo fainali wakiwa vinara wa kundi A
Gomes amesema kutinga robo fainali lilikuwa lengo kuu lakini kilichomfurahisha zaidi ni vile wachezaji wake walivyocheza na kufanikisha kusudio hilo kwa ushindi mnono dhidi ya moja ya timu bora barani Afrika katika muongo huu
"Tuna furaha sana sio tu kwa sababu tumefuzu lakini pia tumecheza mechi nzuri sana. Tungeweza kufunga zaidi sababu tulitawala sana mchezo lakini tumeridhishwa sana kwa kufuzu hatua ya robo fainali na tumemaliza katika nafasi ya kwanza," alisema Gomes
Kocha huyo raia wa Ufaransa ameweka rekodi ya kuipeleka Simba robo fainali bila ya kupoteza mchezo mpaka sasa
Ni Simba na Mamelodi Sundown pekee ndio hazijapoteza mchezo mpaka raundi ya tano ya michuano hiyo
Zote zimejikusanyia alama 13 na zimejihakikishia kutinga robo fainali zikiwa vinara wa makundi yao
Mchezo wa mwisho Simba itaifuata Al Ahly kule Misri, utapigwa wiki ijayo, April 10
Huu ni mchezo wa kukamilisha ratiba tu kwani matokeo yake hayatabadili chochote kwenye msimamo wa kundi