Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amewataka mashabiki kununua tiketi mapema tayari kushuhudia historia nyingine inayokwenda kuandikwa uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita
Baada ya CAF kuiruhusu Tanzania kuingiza mashabiki 10,000 katika michezo yake ya Kimataifa inayopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Manara amesema mashabiki wanapaswa kuchangamkia tiketi mapema kwani hazitauzwa uwanjani
Manara amesema Simba ni lazima ishinde mchezo huo ili kujihakikishia nafasi robo fainali mapema
"Kwa mashabiki wetu watu 10,000 ni watu wachache sana. Hatutarajii siku ya mchezo watu wawe bado hawajanunua tiketi sababu siku ya mchezo CAF hawaruhusu tiketi kuuzwa uwanjani."
"Hakuna namna lazima tupate ushindi kwenye mchezo huu. Hii itakuwa ni DO OR DIE; SEASON TWO na hiyo ndio itakuwa kauli mbiu yetu."
Aidha Manara amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri, nyota wa Kimataifa wakiendelea kuwasili
"Kikosi chetu kipo vizuri wachezaji wengine wameshawasili na wengine wanaendelea kuwasili. Afya za wachezaji zipo vizuri tofauti na zinavyoandikwa baadhi ya sehemu na tutaendelea kuchukua hatua," alisema Manara
Nae Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez amesema mashabiki wanapaswa kuchangamkia fursa hii adimu ambayo klabu ya Simba imepata
"Leo tumepata habari njema kutoka CAF kuwa tumeruhusiwa mashabiki 10,000 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita Club"
"Hii ni fursa ya kipekee ambayo tumeipata. Hakuna timu imeruhusiwa kwa idadi hii. Masharti ni mengi na lazima tuzingatie taratibu walizoweka," alisema Barbara
Viingilio vya mchezo huo Mzunguuko ni Tsh 10,000/-, VIP B ni Tsh 25,000/= wakati VIP A ni Tsh 40,000/-
