Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kumkamata mmoja kati ya washtakiwa watano waliopo nje ya Tanzania wanaodaiwa kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’.
Uamuzi huo umetolewa baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kutaka mahakama kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa huyo anayeishi Afrika Kusini.
Hayo yameelezwa na wakili wa Serikali, Yusuph Abood Alhamisi Machi 25, 2021 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili dereva teksi, Mousa Twaleb (46) ilipotajwa mahakamani hapo.
Twaleb na wenzake watano ambao bado hawajakamatwa, wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kumteka nyara Mo na kutakatisha Sh8 milioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 42/2019.
Abood ameeleza hayo muda mfupi baada ya upande wa utetezi kudai kuwa mteja wao amekaa muda mrefu gerezani akisubiri washtakiwa wengine wakamatwe na hakuna juhudi zozote zinazofanywa na upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa shauri hilo.
Ameieleza mahakama hiyo kuwa Februari 19, 2021 upande wa mashtaka uliwasilisha ombi hilo kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ukiomba mahakama ya Kisutu kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa huyo ambaye amepatikana nchini Afrika Kusini ili aletwe nchini na kuunganishwa katika kesi hiyo