Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes anaweza kuandika historia ya kipekee msimu huu kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika
Akiwa ameiongoza Simba kwenye mechi nne za michuano hiyo, Simba inaongoza kundi A ikiwa imejikusanyia alama 10
Lakini muhimu zaidi, Simba haijaruhusu bao katika nyavu zake ikiungana na Wydad Athletic kuwa timu pekee ambazo zina 'cleansheet' katika michezo yote minne
Gomes amesema amefarijika kwa mafanikio waliyoyapata mpaka sasa hata hivyo amesisitiza bado hawajafikia malengo yao
"Nafurahi kuona tunaongoza kundi A na tukiwa na michezo miwili mkononi. Tutacheza na AS Vita nyumbani na kwenda Misri kumaliza dhidi ya Al Ahly. Nadhani tuna nafasi nzuri sana ya kumaliza vinara wa kundi A," alisema Gomes
"Tukifanikiwa hilo, tunayo nafasi nzuri ya kufika nusu fainali kama tulivyojiwekea katika mipango yetu," Gomes aliuambia mtandao wa Goal
Simba inahitaji alama moja tu kuweza kutinga robo fainali lakini kama itashinda mchezo mmoja na angalau kutoka sare mwingine, itamaliza ikiwa kinara wa kundi A
Faida ya kumaliza kinara wa kundi ni kuwa, kwenye hatua ya robo fainali itacheza na timu iliyomaliza katika nafasi ya pili katika kundi jingine
Lakini pia itaanzia ugenini na baadae kumalizia mchezo wa mkondo wa pili nyumbani