Pamoja na kutopata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere amesema yuko vizuri ndio maana anaendelea kuongoza mbio za kuwania ufungaji bora kwa msimu wa tatu mfululizo
Nyota huyo raia wa Rwanda aliyezakiwa Uganda, msimu huu amefunga mabao 9, akifunga jumla ya mabao 54 katika ligi kuu ya Vodacom ndani ya misimu mitatu
Tangu kuwasili kwa kocha Didier Gomes, Kagere amekuwa na nafasi finyu ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza
Lakini amefanya vizuri kila alipopewa nafasi na haishangazi kuona msimu huu amefunga mabao tisa akiongoza orodha ya wafungaji bora akiwa sambamba na nahodha John Bocco
Mnyarwanda huyo amesema kila kocha ana chaguo lake la kikosi, kutoanzishwa haimaanishi kuwa ameshuka kiwango ndio maana yuko juu kwenye orodha ya wanao ongoza kwa mabao msimu huu
"Sijashuka kiwango, nipo kama nilivyokuwa awali kipindi natumika kikosi cha kwanza, ninaendelaa kujifua kama kawaida, kwani najua hata nikipewa nafasi napaswa kuonyesha uwezo huo," alisema Kagere alinukuliwa na Mwanaspoti
"Unajua kila kocha huwa na wachezaji wake anaotaka kuwatumia kulingana na mechi husika na jambo hilo ndio nakutana nalo kwa kutumika kama mbadala na kuna ambaye anaanza katika kikosi cha kwanza"
"Nina imani mazoezi haya ya nguvu ambayo nayafanya kama nikiwa sijacheza nakuwa nimetumika kama wale wenzangu waliocheza ili kuwa sawa na sijawahi kuona naonewa au kuongea kokote zaidi ya kujiandaa ili nikipewa nafasi niweze kuonyesha ubora. Sitamani kuona kazi yangu kisoka inakwenda chini kirahisi nitapambana na nitacheza kama ilivyokuwa hapo awali, lakini kuhusu suala la kufunga hilo huwa linatokea kama nikipata nafasi ya kucheza mara kwa mara"
"Ukiangalia licha ya kucheza mechi chache bado nipo kileleni mwa ufungaji wa mabao katika ligi msimu huu na bado nina nafasi ya kuongeza, hivyo nahitaji yangu katika mechi yakifika nina imani nitapewa nafasi," alisisitiza Kagere
Gomes hupendelea kuanza na mshambuliaji Chris Mugalu katika kikosi chake cha kwanza huku Kagere na Bocco wakipishana kucheza kutegemeana na mechi