Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Merrrikh, kocha mkuu wa Simba Didier Gomes amesema wanakaribia kufanikiwa malengo yao ya kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa
Ushindi dhidi ya Al Merrikh umeifanya Simba ifikishe alama 10 na kuendelea kubaki kileleni mwa kundi A wakiwa mbele kwa tofauti ya alama tatu dhidi ya Al Ahly yenye alama saba
Kimahesabu, Simba inahitaji alama moja tu kutoka mechi zao mbili zilizobaki ili waweze kutinga robo fainali
Akizungumza baada ya mchezo jana, Gomes alisema ushindi umewaweka katika nafasi nzuri, matokeo hayo yalikuwa muhimu sana kwao
"Ulikuwa ni mchezo mzuri kwetu, tulihitaji ushindi siku ya leo, tumeridhishwa kwa kufunga magoli matatu na kucheza vizuri. Sasa tuna alama 10 na tunaongoza kundi," alisema Gomes
Mchezo unaofuata ni dhidi ya AS Vita na utapigwa April 02 katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Huu ndio mchezo ambao unaweza kuihakikishia Simba kwenda robo fainali kwani ushindi au matokeo ya sare yatatosha
Jana AS Vita walikumbana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Al Ahly, mabingwa watetezi wa michuano hiyo
Hawa safari yao msimu huu inaweza kufikia tamati pale kwa Mkapa kwa mara ya pili kwani wakifungwa au hata sare watakuwa wameondoshwa katika michuano hiyo
Mwaka juzi Simba iliwaondosha katika michuano hii hii kwa kuwafunga mabao 2-1 na Simba kuvuka robo fainali sambamba na Al Ahly
Kuna kila dalili hata msimu huu ni Simba na Al Ahly tena ndio watakaosonga mbele robo fainali