Mechi nyingine ngumu uwanja wa Benjamini Mkapa imemalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 Simba ikichomoa dakika za jioni kujinusuru na kipigo cha pili kutoka kwa Tanzania Prisons
Ulikuwa mchezo mgumu, Prisons wakiingia na 'pira lao la gumu', walimaliza mchezo huo wakiwa na wachezaji pungufu baada ya Jumanne Elifadhili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na mchezo usio wa kiungwana


Katika kipindi cha kwanza, mshambuliaji Chris Mugalu alikosa mkwaju wa penati, pigo ambalo lingeweza kuwapa Simba uongozi
Ni Prisons waliotangulia kufunga kwenye dakika ya 56 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Salum Kimenya
Jitihada za Simba kusaka bao la kusawazisha zilizaa matunda kwenye dakika za lala salama baada ya Luis Miquissone kumalizia mpira wa kichwa ambao mwanzo ulipigwa na Bernard Morrison
Pamoja na kuwa pungufu Prisons walikuwa imara sana katika kujilinda, wanafanikiwa kuondoka na alama nne mbele ya Simba msimu huu
Huu ni msimu wa pili Simba imeshindwa kupata ushindi dhidi ya Prisons kwenye ligi
Mabingwa hao watetezi wameongeza alama moja ambayo sasa inawafanya wafikishe alama 46 na kuendelea kusalia katika nafasi ya pili