Timu ya Soka ya Namungo leo iko Casablanca, Morocco kucheza mechi ya kwanza ya kundi D katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Raja Casablanca ya huko
Namungo kama timu ngeni katika michuano hiyo mikubwa imetinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuindosha Primeiro de Agosto ya Angola katika mchezo wa mwisho wa mtoano kwa jumla ya mabao 7-5.
Aidha, Raja ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondoa US Monastir ya Tunisia kwa penalti 6-5 baada ya kila mmoja kushinda nyumbani kwake bao 1-0 na hivyo, kuwa na bao 1-1.
Wenyeji ni wazoefu katika michuano hiyo waliwahi kutwaa ubingwa wa kombe hilo mwaka 2018 lakini pia, 2019-2020 walifika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Imewahi kufika hatua za juu kwa vipindi tofauti na ni moja ya timu kubwa za Morocco zenye mafaniko makubwa kila msimu. Kwa sasa inaongoza ligi kwa pointi 19 katika michezo tisa ikiwa ni timu pekee haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa.
Ukilinganisha timu hizo mbili kwa ubora kuanzia vikosi vyao Namungo iko chini ila katika mpira lolote linawezekana
Mabingwa wa Tanzania Simba Sc ambao wanaiwakilisha nchi katika michuano ya ligi ya mabingwa, tayari wamedhihirisha kuwa timu zetu zinaweza kupata matokeo ugenini wakiwafunga AS Vita bao 1-0 nchini Congo na kutoka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Al Merrikh nchini Sudan
Namungo Fc wanapaswa kujiamini na kucheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha wanapata matokeo huko Morocco