Jumanne ya March 16 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, mabingwa wa nchi Simba watakuwa na mchezo muhimu wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Merrikh
Huu ni mchezo ambao matokeo ya ushindi yatawasogeza karibu na robo fainali wababe hao wa soka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki
Hata hivyo nyota wawili wa kikosi cha kwanza Paschal Wawa na Thaddeo Lwanga hawatakuwa sehemu ya mchezo huo, wana kadi mbili za njano
Kulingana na sheria za CAF ni kuwa mchezaji anayepata kadi mbili za njano anakosa mchezo mmoja utakaofuata baada ya mchezo wa mwisho alioonyeshwa kadi ya pili
Akizungumzia kukosekana kwa wachezaji hao, Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema atatafuta njia nyingine ambayo itakuwa mbadala na sahihi kwao ili kwenda kucheza katika ushindani ule ule na kupata matokeo mazuri.
Hata hivyo kocha huyo raia wa Ufaransa amesema kwa sasa akili na mawazo yao wameelekeza kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa keshokutwa Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
"Kwa sasa tunakabiliwa na mchezo muhimu wa ligi siku ya Jumatano, mipango yetu tumeielekeza katika mchezo huo kwanza"
"Baada ya mchezo huo tutaanza maandalizi ya kucheza na Al Merrikh. Tutaangalia jinsi gani ya kutayarisha timu ili kuwa na kiwango bora zaidi"
"Tuko nyumbani, mbinu zetu zitakuwa tofauti na vile tulivyocheza ugenini. Wachezaji wangu wote wapo vizuri kukosekana kwa mmoja kuna mwingine ambaye anaweza kuwa mbadala wake na tukafanya vizuri" alisema Gomes