Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez na Kocha Mkuu Didier Gomes wamekanusha kuwepo kwa tofauti kati ya mchezaji Bernard Morrison kama ambavyo taarifa zimeenea kupitia mitandao ya kijamii
Muda mfupi baada ya Simba kurejea nchini ikitokea Ethiopia, Barbara amesema taarifa hizo ni za uongo na hakuna tofauti yoyote kati ya kocha na mchezaji yeyote akiwemo Morrison
"Kwanza nimesikitika kwa kuwa hiyo ni habari ya uongo na ya kutengenezwa, Bernard Morrison alibaki Dar es Salaam kwa sababu za kiufundi"
"Ukianza kutengeneza habari za uongo unamsaidia nani? Simba imetoka kupata sare na pointi moja ugenini. Wangehoji tumejipangaje hadi tunaweza kupata matokeo ugenini? Mwalimu anasemaje? Wachezaji wanafikiria nini?"
"Watu wanahamisha na kutengeneza habari yake, haijengi na nimesikitishwa sana kwa sababu haisaidii timu wala mchezaji. Sio sawa, ni habari ya uongo," alisema Barbara
Nae Kocha wa Simba Didie Gomes amesema hakuna tofauti yoyote kati yake na Morrison, Morrison kuachwa Dar wakati wa safari ya Sudan haimaanishi wana tofauti.
"Morrison ni mchezaji mzuri mwenye kipaji lakini yeye kubaki Dar wakati timu inasafiri kuelekea Sudan haimaanishi tuna tofauti"
"Kuna mambo yake ya kifamilia ambayo siwezi kuyaweka wazi na sababu nyingine zikafanya abaki lakini atajumuika na timu kwa ajili ya mechi zijazo," alisema Gomes