Kocha Mkuu wa klabu ya soka ya Simba, Didier Gomes amesema mchezo wao unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan hautakuwa rahisi kutokana na wapinzani wao kupoteza mechi mbili mfululizo.
Gomes aliyekuwa kocha wa Al Merrikh kabla ya kujiunga na Simba, amesema wapinzani wao hawatakuwa tayari kupoteza mchezo wa tatu katika michuano hiyo lakini nao wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri
"Hautakuwa mchezo rahisi, hii ni timu ninayoifahamu vizuri lakini hata wao wananifahamu. Wamepoteza mechi mbili za mwanzo, mchezo uliopita wakifungwa na AS Vita hapo Sudan"
"Wako kwenye presha kubwa ya kupata matokeo yao ya kwanza, lakini nasi tuko vizuri tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata matokeo muhimu yatakayotuweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata," alisema Gomes
Simba itaondoka jijini Dar es salaam leo jioni, kuelekea Sudan wakipitia Ethiopia tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi, March 06
Siku kumi baadae, March 16 timu hizo zitarudiana jijini Dar es salaam katika mchezo wa raundi ya nne