Baada ya juzi kutinga hatua ya 16-bora ya Kombe la Azam Federation maarufu FA Cup, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, leo watashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha JKT Tanzania katika kinyang'anyiro cha ligi hiyo, huku wakiutumia mchezo huo kujiandaa na mechi ijayo dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan.
Simba ambayo Ijumaa iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon kwenye mechi hiyo ya Kombe la FA, kesho itapanda ndege kuifuata Al-Merrikh kwenye mechi yao ya tatu ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, wataifuata Al-Merrikh wakiwa tayari wameshinda michezo yao miwili baada ya kuichapa AS Vita ya DR Congo bao 1-0 ikiwa kwao kabla ya Jumanne iliyopita kuibuka na ushindi kama huo hapa nyumbani dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema, hesabu zao kwa sasa ni mechi dhidi ya JKT Tanzania kwa kuwa malengo yao kwanza ni kutwaa mataji yote mawili, Kombe la FA na ubingwa wa Ligi Kuu, huku wakifanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gomes amesema katika mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania, ataendelea kufanya mabadiliko ya kikosi chake ili kutoa mapumziko kwa baadhi ya nyota wake.
Amesema ana imani kubwa na kikosi chake na kwamba wachezaji watakaopata nafasi wanaweza kupambania timu kupata matokeo chanya.
"Kwa ujumla ligi imekuwa na ushindani mkubwa, lakini kwetu sisi malengo yetu ni kila mechi kupata matokeo chanya, kwa sasa tunasahau matokeo ya mechi iliyopita na kuelekeza akili yetu kutafuta pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania.
"Tunajua ni mechi ngumu kwa kuwa tunahitaji kupata pointi muhimu ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye mbio za ubingwa, lakini tutapambana," alisema Gomes