Mabingwa wa nchi Simba leo wanaendelea na kampeni ya kutetea ubingwa wao wa ligi kuu kwa msimu wa nne mfululizo watakaposhuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa saa moja usiku
Baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon juzi na kuwashuhudia wababe hao wa soka nchini wakitinga hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), leo watakuwa na nafasi ya kuendelea kusogea kileleni mwa msimamo wa ligi
Simba imekusanya alama 42 katika michezo 18, ni alama saba pungufu ya Yanga inayoongoza ligi ikiwa na alama 49 baada ya kushuka dimbani mara 21
Hata hivyo hesabu ziko upande wa Simba kwani ushindi katika michezo yake mitatu ya viporo, utawashuhudia wakiwaondoa Yanga kileleni mwa msimamo
Kocha Didier Gomes jana alisimamia mazoezi ya mwisho ya kikosi chake akiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi mnono dhidi ya maafande hao kutoka mkoani Dodoma
Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa mkoani Dodoma