Mabingwa watetezi wa michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Simba leo wanatashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mchezo wa mzunguko wanne wa mashindano hayo dhidi ya African Lyon utakaochezwa saa moja usiku.
Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi mapema na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
Gomes alisema mechi zote ambazo timu yake inacheza ni sawa na fainali kwa sababu wanahitaji kukamilisha malengo waliyonayo ya kuchukua mataji.
Mfaransa huyo alisema katika soka hakuna mechi ndogo wala kubwa kwa sababu kila timu hujiandaa kupata matokeo chanya na amejiandaa kukabiliana na ushindani wowote kwenye mchezo huo.
"Kila siku tunakutana na changamoto tofauti, tumesahau matokeo ya mechi iliyopita na sasa akili yetu ni mchezo wa Kombe la FA, tunatarajia kukutana na ushindani hasa kwa sababu ni mashindano ya mtoano, tumejipanga kuendeleza kasi yetu tuliyonayo kwa sababu tunahitaji ubingwa wa michuano hii pia," Gomes alisema.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema wataingia katika mchezo huo kwa 'nguvu kubwa' kuhakikisha wanapata ushindi.
"Tumekuwa na tabia ya kupoteza mechi ndogo baada ya kumaliza mchezo dhidi ya timu kubwa, nimeongea na Matola (Selemani- Kocha Msaidizi) kwa ajili ya kuongeza msisitizo, mimi kwangu ni bora kufungwa 2-0 na Al Ahly, lakini sio African Lyon, tutaingia kwa nguvu ile ile tuliyoishia nayo," Manara alisema.
Aliongeza msimu huu Simba imejipanga kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini lengo kuu ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.