Wakati Simba ikitarajiwa kushuka uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Ijumaa kuikabili African Lyon katika mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Msemaji wa mabingwa hao wa nchi Haji Manara, amewatahadharisha wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha hawadharau mchezo huo
Manara amesema kwa muda mrefu Simba imekuwa na kasumba ya kudharau mechi hasa wanapotoka kushinda mechi kubwa hivyo wanapaswa kujifunza kutokana na makosa ya nyuma
"Imekuwa kama tabia yetu, kwa miaka mingi huwa tukitoka kushinda mechi kubwa, hatufanyi vizuri katika mechi inayofuata. Katika michuano hii ya FA tuliwahi kutolewa na Green Worriors, Mashujaa zote kutoka daraja la kwanza"
"Nimemkumbusha kocha Msaidizi Selemani Matola kuhusu kasumba hii, wao kama benchi la ufundi wawakumbushe wachezaji kuwa wanasimba hawatakuwa tayari kuona timu yao inafungwa na African Lyon"
"Ni bora tungefungwa na Al Ahly kuliko African Lyon kesho. Sisi lengo kuu la msimu huu ni kushinda ligi kuu na kombe la FA, kule michuano ya ligi ya mabingwa malengo yetu ni kutinga robo fainali, tukifika nusu fainali itakuwa mafanikio zaidi," alisema Manara
Mchezo dhidi ya African Lyon ni wa raundi ya nne michuano ya kombe la FA (ASFC) na utapigwa kuanzia saa moja kamili usiku