Kocha Mkuu wa Al Ahly Pitso Masemane amesema anafahamu wanakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba uwanja wa Benjamin Mkapa hapo kesho
Mosimane anayetizamwa kuwa kocha bora barani Afrika, amesema anafahamu uimara wa kikosi cha Simba huku akikiri kushitushwa na ushindi ambao Simba wamepata kule Dr Congo kwa kuifunga AS Vita bao 1-0
"Nafahamu hautakuwa mchezo mwepesi. Naifahamu Simba, ni timu yenye wachezaji wazuri. Luis (Miquissone) ni mchezaji hatari sana, namfahamu kwani nilikuwa nae wakati niko Mamelodi Sundowns ni mimi niliyemtoa kuja Simba. Ni mchezaji hatari sana. Yule mshambuliaji anayevaa jezi namba saba (Mugalu) na yule namba 14 (Kagere) ni wachezaji wenye kiwango cha juu sana"
"Nafahamu nguvu ya Simba wakiwa nyumbani ni mashabiki wao. Ni timu inayoendeshwa na mashabiki, ni hatari kucheza na timu ya aina hii hasa pale wanapopata kasi dimbani. Pia nafahamu ni timu inayocheza soka zuri la kuvutia. Hivyo hautakuwa mchezo mwepesi," alisema Mosimane
Akizungumzia kikosi chake, Mosimane amesema wamelenga kupata matokeo ya kuwawezesha kufuzu hatua ya robo fainali mapema kuepuka presha ya mechi za mwishoni
"Msimu uliopita tulilazimika kusubiri mchezo wa mwisho kabisa dhidi ya Al Hilal tuweze kufuzu. Hatupendi jambo hilo litokee msimu huu hivyo lengo letu ni kukusanya alama mapema"
Mapema kocha msaidizi wa Simba Selemani Matola alisema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali
Matola alisema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo na hakuna majeruhi
"Tunajua tunaenda kukutana na timu bora barani Afrika. Hilo halitusumbui kwani tumefanya maandalizi mazuri tukilenga kushinda"