Mabingwa wa nchi Simba jioni ya leo watashuka uwanja wa Karume, Musoma kuikabili Biashara United katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Wakiwa wametokea kule DR Congo walikofanikiwa kuiangusha AS Vita, Machampioni hao wa Taifa, wamepania kuendeleza wimbi la ushindi
Hata hivyo wanakutana na timu ambayo imekuwa ngumu sana kufungwa katika uwanja wake lakini Simba imejipambanua kwa kuwa safu bora ya ushambuliaji
Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo ambao hesabu zao ni kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu
"Tupo tayari kupambana na tupo tayari kutoa kila tulichonacho. Biashara ni timu nzuri na inacheza mfumo mzuri lakini tupo kwenye hali nzuri ya kujiamini na hasa baada ya ushindi wa DR Congo. Tunahitaji alama hizi tatu ili kusogea kileleni," alisema Gomes baada ya mazoezi ya kikosi chake yaliyofanyika uwanja wa Karume jana jioni
Baada ya mchezo huo Simba itarejea jijini Dar es salaam kujiandaa na raundi ya pili ligi ya mabingwa, wakitarajiwa kuikabili Al Ahly Februari 23