Mabingwa wa nchi Simba wanatarajiwa 'kupaa' kwenda jijini Mwanza na baadae kuunganisha mkoani Mara kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Biashara United ambao utapigwa keshokutwa Alhamisi
Baada ya kuiwakilisha vyema nchi kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita katika mchezo wa ligi ya mabingwa kundi A, Simba wanakwenda Musoma wakiwa na hesabu za kuondoka na alama zote tatu
Huu ni mchezo wa pili baina ya timu hizo msimu huu Simba ikifanikiwa kushinda mabao 4-0 katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam
Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema lengo kuu ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuendelea kuwapa presha vinara wa ligi hiyo Yanga ambao kimahesabu wanaweza kuwashusha kileleni kama watashinda mechi zote za viporo
Gomes amesisitiza kuwa wanahitaji kutetea ubingwa kwa msimu wa nne lengo likiwa kupata nafasi nyingine ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa
Baada ya kurejea kutoka DR Congo, nyota wa Simba walipewa mapumziko ya siku moja na baadae kuanza maandalizi ya mchezo huo