Wakati kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba kikitarajiwa kuwasili mchana wa leo wakitokea DR Congo ambako walipata ushindi wa kihistoria kwa kuichapa AS Vita bao 1-0 katika mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya makundi, uongozi wa machampioni hao wa nchi umewataka mashabiki wasiende kuwapokea uwanja wa Ndege badala yake waendelee na shughuli zao
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Haji Manara amesema ushindi walioupata Congo ni mwanzo tu, bado kazi hawajaimaliza hivyo hawapaswi kuanza kusherehekea sasa
"Tumepokea salamu nyingi za ushindi ila mashabiki kwa sasa tunawashukuru sana kwa sapoti yao, kuhusu kutupokea kwa furaha bado, watuache kidogo bado kazi ni ndefu"
"Hatujafikia malengo yetu, ikifika wakati tunarudi na ubingwa, mataji pale na mambo mengine itakuwa rasmi kwa mashabiki kuja ila kwa sasa tunawaomba mashabiki muendelee na shughuli zenu, tunajua mnafurahi kuona tumeshinda nasi tunafuraha ila malengo yetu bado na safari bado ni ndefu," alisema Manara
Simba iliondoka DR Congo mapema jana ambapo wamelala nchini Ethiopia leo asubuhi msafara ukiondoka nchini humo kurejea Tanzania