Wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba leo wanakianza kibarua cha kupigania pointi tatu dhidi ya AS Vita ya Congo DR kwenye mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya michuano hiyo
Mchezo huo wa kundi A utachezwa saa 4:00 usiku kwenye uwanja wa taifa wa nchi hiyo wa Martyrs of Pentecost uliokuwa unajulikana zamani kama Kamanyola uliopo Kinshasa.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka juzi hatua kama hiyo ambapo Simba wakiwa ugenini walipoteza kwa mabao 5-0 na kisha mechi ya marudiano nyumbani kwenye uwanja wa Mkapa wakashinda mabao 2-1
Ulikuwa ni mchezo wa mwisho wa kuamua nani asonge mbele kwa pointi na ndipo Simba ikasonga.
Leo zinakutana tena zikiwa na tofauti kidogo kuanzia wachezaji, benchi la ufundi kwa hiyo wote watakuwa wameboresha vikosi vyao lakini wakiwa katika viwango tofauti.
Kuna wachezaji kama Jean Makusu, Tuisila Kisinda, Tonombe Mukoko na wengine hawapo tena katika kikosi cha Vita wakiwa wamewauza na kununua wengine ila kocha wao ni yule yule Florent Ibenge.
Na kwa Simba kuna wachezaji kama James Kotei, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi hawapo kikosini ila asilimia kubwa wapo isipokuwa Kocha Didier Gomez ambaye ni mpya ni baadhi ya wachezaji waliosajiliwa. hivi karibuni
Simba ambao ni mabingwa mara tatu wa Ligi Kuu Bara, wapo katika kiwango kizuri baada ya kuonesha ubora katika michezo iliyopita hatua za awali ikiwatoa FC Platnum kwa mabao 4-1. Mchezo wa kwanza walifungwa 1-0 ugenini kisha wakashinda 4-0 nyumbani.
Mchezo mwingine waliwatoa Plateau United ya Nigeria na kutinga hatua hiyo kwa jumla ya bao 1-0 baada ya mchezo wa kwanza kushinda ugenini 1-0 na kupata suluhu nyumbani.
Timu hiyo inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kwa pointi 39 katika michezo 17 iliyocheza. Michezo yake ya mwisho ya ligi ilishinda dhidi ya Dodoma jiji mabao 2-1 na kupata sare dhidi ya Azam FC ya mabao 2-2.
Wekundu hao wa Msimbazi wapo vizuri zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ikiongoza kwenye ligi kwa kufunga mabao 41 mengi kuliko timu nyengine na mshambuliaji wake hatari zaidi ni Medie Kagere anayeongoza kwa kufunga mabao tisa, Cletus Chama akiwa na pasi za mabao tisa na mabao sita, akifuatiwa na Luis Miquissone pasi nane na mabao mawili
Kwa upande wa Vita iliyocheza raundi moja ilimtoa Young Buffaloes ya Mbabane kwa jumla ya mabao 6-3, mchezo wa kwanza wakitoka sare ugenini mabao 2-2 na kushinda mabao 4-1 nyumbani.
Katika ligi ya kwao wanashika nafasi ya pili kwa pointi 32 katika michezo 14 wakiwa hawajapoteza mchezo
Ni mchezo ambao Simba inaweza kupata matokeo ugenini kama kocha Didier Gomes atazichanga karata zake vyema kwani ana kikosi imara