Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez amesema wachezaji leo wanapaswa kupambana kuhakikisha timu inapata ushindi na kuanza vyema michuano ya ligi ya mabingwa hatua ya makundi
Saa nne usiku Simba itashuka Stade de Martyrs pale Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuikabili AS Vita katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi
Barbara amesema wamewaahidi wachezaji bonus nono kama watapata ushindi leo lakini pia michuano hii ni nafasi kwao kujitangaza kwani inafuatiliwa kote duniani
"Kama viongozi tumezungumza na wachezaji kuwaeleza umuhimu wa mchezo huu. Ukiachilia ahadi ya bonus tuliyowapa kama watashinda, lakini tumewaambia michuano hii ni nafasi kwao kujitangaza. Kuna Mawakala kutoka kila kona ya dunia wanaifuatilia. Hili ni dirisha zuri kwao kuonekana," alisema
Aidha Barbara amesema kwa upande wa uongozi wametimiza wajibu wao kwa kuhakikisha benchi la ufundi na wachezaji wanakuwa na mazingira mazuri kuelekea mchezo huo
Hivyo sehemu iliyobaki ni wajibu wao kuhakikisha wanawapa furaha Mamilioni ya Mashabiki wao ambao watakuwa wakifuatilia mchezo huo