Kikosi cha Simba kinatua leo DR Congo kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita utakaopigwa Ijumaa
Kufuatia mafanikio waliyoyapata mwaka juzi katika michuano hiyo, Simba wamekuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Congo
Katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu wa 2018/19 Simba ikiwa kundi moja na AS Vita pamoja na Al Ahly, walifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili na kutinga robo fainali
Simba ilishinda mechi zake zote jijini Dar es salaam ikizifunga JS Soura 3-0, Al Ahly 1-0 na AS Vita 2-1
Vita bado wanaweweseka na kipigo katika michuano ile licha ya kuwa wao walishinda mabao 5-0 katika mchezo wa kwao
Baada ya kuiona Simba katika michuano ya Simba Super Cup, AS Vita wanajua miamba hao wa soka kutoka Tanzania sasa wana kikosi imara zaidi kuliko mwaka juzi
Aidha uwepo wa wachezaji mahiri kama Luis Miquissone, Larry Bwalya na Clatous Chama ni sababu nyingine ya Wacongomani hao kuwa na hofu
Wachezaji kama Bernard Morrison na Chris Mugalu wanawafahamu vizuri kwani kwa nyakati tofauti wamewahi kucheza ligi kuu ya DR Congo
Morrison amewahi kucheza hapo AS Vita na klabu ya DC Motema Pembe wakati Mugalu yeye alicheza FC Lupopo, hawa hapo Congo ni kama wamerudi nyumbani
Aidha kipigo cha mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki waliocheza karibuni, kimewatia hofu zaidi mashabiki wa AS Vita ambao wanafahamu mambo yanaweza kuwaharibikia mbele ya Simba inayonolewa na kocha Didier Gomes ambaye ana uzoefu na michuano hiyo