Kibarua cha kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes ni siku ya kesho Alhamisi pale uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma wakati kikosi chake kitakaposhuka dimbani kuikabili Dodoma Jiji katika mchezo wa kiporo ligi kuu ya Vodacom
Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi kwa Gomes ambaye tayari ameiongoza Simba kushinda taji la michuano ya Simba Super Cup iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita
Gomes amesema wanahitaji kushinda mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ili waendelee kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga inayoongoza ligi
"Utakuwa mchezo mgumu lakini tupo tayari kupambana ni muhimu sana. Tuna michezo mitatu mkononi na tunatakiwa kushinda michezo yote ili kupunguza alama na timu iliyopo kileleni na mchezo wa kwanza ni kesho,"alisema Gomes
Simba ilijifua uwanja wa Jamhuri jioni ya leo tayari kwa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Simba mkoani Dodoma





