Ubora wa kikosi cha Simba hasa baada ya kushusha majembe ya kazi ikiwemo Mzimbabwe Tatenda Perfect Chikwende, na kurudi kwa makali ya, Bernard Morrison kumemshtua kocha wa Azam, George Lwandamina ambaye amelazimika kujipanga kivingine kuelekea mchezo baina ya timu hizo utakaopigwa Jumapili ijayo kunako uwanja wa Benjamin Mkapa.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Simba na Azam kukutana msimu huu ukiwa sehemu ya michezo ya viporo vya mzunguko wa kwanza wa ligi.
Kumbukumbu ya mwisho ya timu hizo kukutana ni ushindi wa mabao 3-2 walioupata Simba Machi 4, 2020 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili msimu uliopita
Akizungumzia kuhusu maandalizi yao kuelekea mchezo huo, Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ amesema timu yao inahitaji kujiandaa vyema kuweza kuikabili Simba
"Kikosi chetu kinaendelea na mazoezi kujiandaa na michezo ya mzunguko wa pili wa ligi, tulianza baada ya kukamilika kwa michuano ya Mapinduzi ambapo tulicheza michezo mitatu ya kujipima nguvu.
"Kati ya michezo hiyo tulishinda michezo miwili na kupoteza mchezo mmoja, kabla ya kucheza tena dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam.
"Michezo hii ni sehemu ya maagizo ya kocha Lwandamina ambaye kwa kutambua ugumu wa mchezo wetu dhidi ya Simba utakaopigwa Februari 07, ameomba kupatiwa michezo mingi ya kujipima nguvu ili kukifanya kikosi chake kiwe tayari kwa mchezo huo
"Tunajua Simba wana kikosi kizuri na wameongeza nguvu kupitia usajili lakini hata sisi tumesajili na tumejipanga vizuri," alisema Zakazakazi
Azam Fc wameomba mchezo wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa baadae leo uwanja wa Azam Complex
Kabla ya kukutana na Azam, 'Mnyama' anaanzia mkoani Dodoma kwa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa Alhamisi